Waziri Mchengerwa azindua zoezi la kitaifa la kusaka na kuibua vipaji "mtaa Kwa mtaa."

 



Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni,  Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Oktoba 16, 2022 amezindua  zoezi la  kitaifa la  kuibua na kusaka vipaji  vya Sanaa la "Mtaa kwa Mtaa" eneo la  Ikwiriri wilayani Rufiji, zoezi ambalo litafanyika nchi nzima.

Akizindua zoezi hilo katika eneo la Ikwiriri, Mhe. Mchengerwa amesema eneo linalofuata baada ya uzinduzi wa leo ni Mkoa wa Arusha ambapo litafanyika kila mtaa ili kuibua vipaji kwenye sanaa.

Amewataka watanzania  wenye vipaji vya Sanaa kujitokeza wakati wa zoezi hilo likiendelea  ili waweze kuendelezwa baada ya kuibuliwa, huku akisisitiza  kauli ya Kipaji chako ndiyo mtaji wako.


"Ndugu zangu hii ni ndoto ya Mheshimiwa Rais wetu, Rais anatamani kuona misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ya kuthamini na kuendeleza Sanaa inaendelezwa ili kuwanufaisha vijana" amesisitiza,  Mhe. Mchengerwa
 
Amezitaka mamlaka za wilaya na mikoa kote nchini kusaidia  kuibua  vipaji vya watanzania ili azma ya Serikali  ya kuibua na kuendeleza vipaji vya sanaa iweze kutimia.


Amezihakikishia mamlaka hizo kuwa  Wizara ipo tayari wakati wowote kwa wilaya iliyo tayari kuibua vipaji vya Sanaa.

Mtendaji Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana amesema  zoezi hilo limefanyika kwa siku mbili limeibua vipaji vingi ambavyo vinakwenda kuendelezwa.


Katika zoezi hilo ambalo limekuwa na mafanikio makubwa kutokana na wasanii wengi wa Sanaa mbalimbali kujitokeza lilishirikisha viongozi wa Mashirikisho yote ya Sanaa, Baraza la Sanaa kutoka Zanzibar na wadau mbalimbali wa Sanaa.

Akitoa ushuhuda wa hazina ya vipaji vya Sanaa  katika Wilaya ya Rufiji mbele ya Mhe. Mchengerwa, Rais aliyewakilisha Shirikisho la Muziki nchini, Mzee Yusufu amesema amefurahishwa na  msanii mwenye umri mdogo (11) Musa Mbonde mwenye kipaji kikubwa cha kuimba ambaye amepatia jina la Mzee Yusufu Junior na kuahidi kumsaidia.
Miongoni mwa Sanaa zilizopitiwa ni pamoja na upishi, ngoma, uigizaji, uchongaji na  usukaji kwa zaidi ya wasanii 80 katika wilaya ya Rufiji.

Wakisoma risala mbele ya Mhe. Waziri, wasanii wa Wilaya hiyo wamemwomba   kupatiwa kituo cha redio, studio na vifaa vya kupigia picha ambapo Mhe. Mchengerwa amesema kuwa atafanyia kazi.


Mhe. Mohamed Mchengerwa pia amekakuqua kazi mbalimbali za Sanaa na  kutoa vyeti vya pongezi Kwa wasanii mbalimbali walioibuliwa.

Comments

Popular posts from this blog

TANZANIA KUSHIRIKI KOMBE LA DUNIA-MHE MCHENGERWA

Diamond apongeza Serikali ya Rais Samia kwa kuwasaidia wasanii, kurejesha tuzo