MCHENGERWA AITAKA COSOTA KUTOA ELIMU YA KANUNI MPYA ZA ADA ZA VIBEBEA KAZI ZA SANAA NA MAKAMPUNI YA WASANII
Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameitaka Taasisi ya Hakimiliki nchini (COSOTA) kutoa elimu ya kutosha kwa wadau hususan wabunge kuhusu mabadiliko makubwa yanayofanywa na taasisi hiyo ya kimuundo na kisekta ili kusaidia kuinua maisha ya wadau wa sekta ya Sanaa nchini.
Waziri Mchengerwa ameyasema haya leo Septemba 14, mara baada ya kupitishwa yeye na Naibu wake Mhe, Pauline Gekul na Menejimenti ya taasisi hiyo kwenye kikao cha kujadili rasimu ya kanuni ya uanzishwaji wa Ada kwa vibebea kazi za ubunifu (blank device) na uanzishwaji wa makampuni binafsi ya wasanii ya ukusanyaji na ugawaji mirahaba (CMO).
Amewataka kuharakisha mchakato wa kukamilisha rasimu hizo ili zisainiwe na kuanza kutumika mara moja hatimaye wasani na wadau mbalimbali wa kazi za Sanaa waweze kunufaika na kazi zao.
"Harakisheni, ninakwenda kuisaini kanuni hizi mara moja ili wasanii wafaidi matunda ya kazi zao na kuwaondolea kilio cha muda mrefu." Amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Ameongeza kuwa maendeleo ya teknolojia yamepelekea matumizi binafsi ya kazi bila ruhusa ya wamiliki kwa kuwa ni ngumu kusimamia ( control) kuyapa leseni ( lisensing) na kuyazuia ( banning) hali inayowakosesha mapato makubwa.
Aidha amesema kanuni hiyo inakwenda kuwa mwarobaini wa changamoto hizo za awali.
Kwa upande wa kanuni ya uanzishwaji wa makampuni binafsi ya wasanii ya ukusanyaji na ugawaji mirahaba (CMO) amesisitiza kuzingatia suala la utatuzi wa kisheria wa migogoro kwa wanachama pindi ikitokea.
Aidha amesema kwa kuwa tayari taasisi hiyo imeshaunda mifumo ya kielektroniki ni vema ikaboreshwa na kujumuisha mahitaji ya sasa ili kudhibiti rushwa na upendeleo katika makampuni hayo.
Mara baada ya kukamilika wasilisho hilo linatarajiwa kupelekwa kwenye Kamati ya kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Comments
Post a Comment